‘Kutoka Canvas kwenda Digitali’ | Dar es Salaam, Tanzania
Emergent Art Space is delighted to publish here in Swahili the article about the workshop ‘Kutoka Canvas kwenda Digitali’ which we featured on this site on January 20.
Wachoraji wa sanaa za uoni washauriwa kutumia teknolojia kuwa washindani, kuendeleza nchi.
Wachoraji wa sanaa za uoni Tanzania wameshauriwa kutumia ujuzi wao kulinda na kutunza mila na utamaduni wa nchi na hivyo kuchangia kufikiwa kwa maendeleo endelevu.
Wito huo umetolewa wakati wa warsha ya siku mbili iliyoitwa ‘Kutoka Canvas kwenda Digitali’ iliyoendeshwa jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Warsha hiyo ni sehemu ya mradi wa ‘Hapo Zamani za Kale’ unaolenga kutunza na kuendeleza utamaduni wa asili wa Mwafrika wa kusimulia hadithi kwa kutumia njia za kisasa za sayansi na teknolojia kwa kutumia vitabu vya watoto, na kuchora miongoni mwa nyingine.
Mradi wa 'Hapo Zamani za Kale' unatekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la 'Aqua Farms Organization' (AFO) kwa ufadhili wa shirika la Voice Global.
Akiongea wakati wa kufunga warsha hiyo, mmoja wa watayarishaji wa mafunzo hayo, Elizabeth Mwambulukutu alisema wasanii hao wachoraji wa sanaa za uoni wana nafasi muhimu katika kuitangaza Tanzania duniani, kuhifadhi sanaa na utamaduni wetu kwa vizazi vijavyo na kuelimisha watoto kupitia sanaa hizo kwani watoto huweza kuelewa haraka na kukumbuka walichojifunza kupitia michoro na kuongeza ubunifu.
“Kukua kwa teknolojia kunatoa nafasi kubwa kwa sanaa hizi kuchangia maendeleo ikiwemo kuhifadhi tamatuni zetu na kazi za sanaa” alisema, na kuongeza kuwa “tungependa kuwahamasisha wanawake na walemavu kushiriki kwa wingi katika eneo hilo la sanaa za uoni , hata wale wachanga.”
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wa kidigitali kwa vitendo wasanii ili waweze kuwa washindani katika karne ya 21, na pia kuwafungulia milango ya mafanikio kwa kuwataarifu kuhusiana na fursa mbalimbali zilizopo katika soko kitaifa na kimataifa.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na jumla ya washiriki 16 ikiwa ni pamoja na wasanii wa kazi za mikono, wadau kutoka mradi wa Hapo Zamani za Kale na AFO pamoja na mtaalamu wa lugha za alama kutoka Umoja wa Wataalamu wa Lugha za Alama Tanzania (TASLI).
Wasanii hao waliopatikana baada ya kushindanishwa walijumuisha wanaume watatu na wanawake watatu kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Iringa na Tanga.
Katika mafunzo hayo, msanii maarufu wa katuni, maarufu kama Masoud Kipanya aliwaongoza kwa vitendo wasanii hao sita namna mpya ya kufanya kazi zao tofauti na njia za asili za kuchora walizozowea.
Mmoja wa waanzilishi wa mradi wa Hapo Zamani za Kale, Annastazia Gura alisema bado wasanii wa Afrika wanatumia njia za asili katika kufanya kazi zao. Hali hiyo, alisema, inasababisha wasanii kuachwa nyuma katika zama hizi za teknolojia na kuwa kikwazo katika kuchangamkia fursa na kuwa washindani wa kweli.
Pia, ilibainika kuwa wasanii hasa wachoraji kwa sasa wanategemea aina ya soko moja tu la watalii na hivyo kusababisha vipato vyao kuwa finyu.
“Bado wasanii hapa nyumbani hawana fursa za kujifunza toka kwa wale waliofanikiwa kutokana na ubunifu wao,” alisema Bi. Gura.
Bi. Gura alisema tayari maendeleo ya teknolojia yanaendelea kusababisha mabadiliko makubwa katika sekta nyingine na kwamba wakati umefika kwa wasanii kufaidika pia.
“Tunaona warsha hii ya mafunzo kama njia bora ya wasanii kupata ujuzi mpya na kubuni namna mpya za kukuza vipato,” alisema.
Mbali na wasanii hao kukutana na Masoud Kipanya, mafunzo hayo pia yalikuwa ni nafasi kwo kukutana na kubadilishana uzoefu, kukuza ujuzi kwa kutumia teknolojia na kukuza mtandao baina yao.
Masoud Kipanya alielezea umuhimu wa wasanii wa Tanzania kuwa tayari na wepesi wa kubadilika kuendana na maendeleo ya teknolojia. Alisema: “Kama wasanii ni muhimu kusoma alama za nyakati, lazima tujifunze kubadilika kama vinyonga.”
Mmoja wa washiriki, Jennifer Msekwa alisema: “Kama wasanii wa kisasa, tunatakiwa kujifunza mbinu nyingi ili kuweza kushindana katika ulimwnegu wa sasa wa sayansi na teknolojia.”
Masoud alifafanua zaidi kuwa tofauti na njia za asili za kuchora, matumizi ya teknolojia humpa nafasi kubwa msanii kuboresha kazi yake, kuwa na ubora zaidi na kuokoa muda.
Albano Sylvester, mshiriki mwenye ulemavu katika mafunzo hayo alielezea furaha yake baada ya kupata msaada wa mtaalamu wa lugha ya alama na hivyo kushiriki kikamilifu kama wenzake.
Mwisho
Elizabeth Mwambulukutu is a development communications practitioner and an award winning visual artist committed to shaping the African narrative. She serves as the Regional Communications Manager for WaterAid in East Africa. Elizabeth is driven to advancing Tanzania's creative industry through the restoration, preservation and promotion of authentic African stories. Elizabeth is the co-founder of Arts and Culture for Development Africa (AC4D) and the creative mind behind Elle Emmanuel Photography. She's a Mandela Washington Fellow, Vice Curator for Arusha Global Shapers and Fellow of the Young and Emerging Leaders Project, an initiative of the LéO Africa Institute.